miércoles, 25 de octubre de 2017

JOTO LA KARIAKOO DERBY OCTOBER 28 UWANJA WA UHURU JIJINI DAR ES SALAAM

NGAO+PIC

Milango ya saa 10:00 jioni jumamosi ya Octoba 28, 2017 wapinzani wa jadi nchini katika soka wanakwenda kukutana ndani ya uwanja wa Uhuru katika mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu Tanzania bara . Hawa si wengine bali ni mnyama Simba SC na wana jangwani Yanga SC.


Mchezo huo ni namba tatu Afrika kwa umaarufu katika soka ukitanguliwa na vinara Al Ahly dhidi ya Zamaleki pale jijini Cairo nchini Misri al maarufu kama Caira Derby . Mtanange wa wababe wa ligi kuu nchini Afrika kusini katika viunga vya Soweto Orlando pirates na Kaizer chiefs wanashika namba mbili wakisimama na jina la Soweto derby.
Timu hizi zinakutana huku kila mmoja akiwa na ari, nguvu na hamasa kubwa ya kusaka ushindi ili kujitengenezea njia ya kulinyakua kombe la ligi kuu msimu huu pia kuweka heshima kwa mtani wake. Wote wana wana alama 15 kileleni mwa msimamo wa ligi kuu lakini Simba SC akiongoza jahazi kutokana na wingi wa magoli . Hili peke yake linaleta mvuto wa aina yake kuelekea mchezo huo.
SIMBA SC
Kuelekea mchezo wa jumamosi, wanaonesha hamasa kubwa ya kuibuka wababe katika mtanange huo wa jadi . Upana wa kikosi chao , uwezo wa mchezaji mmoja mmoja , matokeo ya nyuma, uongozi katika ligi vitawafanya kusimama mbele ya Yanga wakiwa na mtaji mzuri wa kisaikolojia kuliko wapinzani wao na endapo wataitumia vyema fursa hiyo wanaweza kuibuka washindi jumamosi.
Msimu huu wa 2017-18 Simba wamefanya usajili mzuri tofauti na misimu kadhaa nyuma toka waliponyakua kombe la ligi kuu kwa mara ya mwisho mwaka 2012. Timu imekuwa na mseto mzuri wa vijana na wakongwe hali inayowafanya kuwa na kikosi kipana kuliko timu yoyote ndani ya ligi kuu kwa sasa . Upana wa kikosi chao ni uwezo unaoshabihana wa mchezaji mmoja mmoja katika kila eneo uwanjani hali inayolifanya benchi la ufundi la timu hiyo kuwa na nafasi kubwa ya kuipanga timu kulingana na mahitaji kwa mchezaji husika pia kutokuwa n hofu ya majeruhi au kuporomoka kwa kiwango cha mchezaji kuhatarisha ufanisi wao.
Mchezo wa mwisho wa Simba SC dhidi ya Mji Njombe walinzi wa kati walisimama Juuko Murshid na Jamali Mlipili aliesajiliwa msimu huu tokea Mbao FC . Akicheza mechi yake ya kwanza ndani ya jezi ya Simba, Mlipili alionesha uwezo mkubwa pembeni ya beki kisiki wa timu ya taifa ya Uganda nafasi ambayo mara nyingi husimama Method Mwanjali na Salimu Mbonde ambaye ni majeruhi. Hii ndio dhana ya upana wa kikosi .
Simba ina wachezaji ambao wana uwezo mkubwa kuamua matokeo ya mechi, kusimama vyema na mfumo na mbinu za mwalimu ili kuipa matokeo chanya timu hiyo endapo bahati ya ushindi itakuwa upande wao.
Ni dhahiri Aishi Manula golikipa namba moja wa timu hiyo na timu ya taifa atakaa langoni siku ya jumamosi Mungu akimjalia afya njema na utimamu wa mwili. Huyu ni golikipa bora wa ligi kuu nchini mara mbili mfululizo na tayari ana uzoefu wa joto la mechi hii akisimama imara langoni mechi ya ufunguzi wa ligi ya Ngao ya jamii dhidi ya Yanga . Manula alipangua penati Kelvin Yondani na kujipanga vyema langoni hali iliyomfanya Juma Mahadhi kujikuta anapaisha mkwaju wa penati na kuwapa ubingwa Simba SC hivyo anaiendea mechi hiyo akiwa vyema kisaikolojia dhidi ya Yanga pia anawajua vyema toka akiwa Azam FC akiwa sehemu ya kikosi kilichoipiga Yanga 4-0 katika mchezo wa Nusu fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu.
Erasto Nyoni ni mchezaji mkongwe ndani ya ligi kuu Tanzania bara na huyu nina imani katika note book ya kocha mkuu wa Yanga SC George Lwandamina lazima yumo kuelekea mchezo huo adhimu kisoka nchini. Erasto ni kiraka eneo lote la ulinzi pia akiwa na uwezo mkubwa kucheza kama kiungo mkabaji. Sifa kubwa mchezaji huyu ni uwezo wa kudumu na kiwango chake ndani ya dakika 90 akicheza kwa kujituma , nguvu , akili ya mpira na kutimiza vyema majukumu yake uwanjani. Akipangwa kama mlinzi wa pembeni basi husimama imara kama mlinzi wa wing pia kiungo wa akiba wa pembeni kulinda n kushambulia. Uwezo wake huo ndio ulimfanya mechi ilyopita dhidi ya Njombe mji kuitengenezea magoli Simba kupitia wing ya kulia akicheza kama mlinzi wa kulia na kiungo wa pembeni. Ana uwezo mkubwa kuibana timu pinzani katika mashambulizi yake ya upande lakini pia akishirikiana vyema na wenzake kupandisha vyema timu . Endapo atapangwa jumamosi beki ya kulia , na benchi la ufundi la Yanga SC kumpanga Mwashiuya kama walivyofanya mechi ya juzi dhidi ya Stand United ni dhahiri kutakuwa na upinzani mkali . Kama Mwashiuya asipokuwa makini kwenye pressing atajikuta mipira mingi anaipoteza kabla ya kupiga krosi au kuukata uwanja . Mechi na Stand walikuwa wakifanya tactical overlapping na Ibrahim Ajibu pale ambapo Mwashiuya akipata mpira alikuwa akikokota kwa kuukata uwanja na Ajibu kutanua pembeni kitu ambacho Erasto ni mkongwe anaweza kuziba njia kwa kusogea juu kwenye edge ya 18 kuziba njia huku akifanya mawasiliano mazuri na walinzi wa kati kwa ajili aidha ya offside trick au covering.
Wengine ni Ally Shomari pia mlinzi wa kulia ambaye anaweza pia kuanza na kusimama vyema katika mechi hiyo , Zimbwe jr kushoto bado ni mwiba mkali katika ulinzi na kupandisha mashambulizi amecheza zaidi ya mechi tano za watani wa jadi hivyo hana pressure . Mkongwe Method Mwanjali kuna uwezekano mkubwa kuanza mechi hiyo akisimama na Juuko. Ana uwezo mzuri sema jazba na hasira za haraka ni kitu cha kuchunga kwake.
Safu ya kiungo ya Simba ndio eneo ambalo Yanga wanatakiwa kulipigia hesabu za mbali kidogo . Hapa ndipo patakapoamua matokeo ya jumamosi aidha sare , kufunga au kufungwa. Msimu uliopita Simba ilikuwa bora eneo la kiungo lakini wakawa butu kwenye safu ya ushambuliaji kwa sababu walikosa mtu wa kuiunganisha timu toka eneo la kiungo kwenda mbele .
Katika soka timu ikiwa bora kwenye ulinzi na kiungo ukaona inapwaya kwenye ushambuliaji kwa maana ya kushindwa kutumia nafasi wanazotengeneza ni dhahiri inamkosa namba 10 ( playmaker ) mwenye uwezo wa kuunganisha kazi za viungo wa kati na pembeni ( technical link up ) kumzunguka mshambuliaji wa kati au kuitanua vyema safu hiyo ili iwe na uwezo wa kutengeneza washambuliaji zaidi ya wawili inapoingia kwenye final third . Ujio wa Emanuel Okwi umetibu vyema tatizo la Simba SC katika hili ndio maana wana uwezo mkubwa wa kufunga . Okwi anasimama kama playmaker na mshambuliaji wa timu hiyo kitu ambacho kinawapa wakati mgumu wapinzani wake .
Si kwamba Omog anatengeneza mfumo wa ushambuliaji wa Simba kumzunguka mchezaji huyo , hapana kiufundi hili ni hatari na kwa uwezo wa kocha huyo sizani kama anaweza kufanya hivyo kwa maana anatambua akibanwa mchezaji huyo patterns zake zinakuwa zimefeli. Mechi na Mji Njombe alimpanga Mzamiru Yassin namba 8 kama kiungo wa juu akicheza sambamba na Jonasi Mkude huku Haruna Niyonzima akicheza wing ya kushoto na Okwi akicheza kama ‘ false 10’ . Kuna mbinu alikuwa anaijaribu Omog kuelekea mchezo wa jumamosi kupitia Njombe mji na kwa kiasi alifanikiwa . Aliwahadaa Mji Njombe kumchezesha Mzamiru kama kiungo mchezeshaji lakini alimpanga kama kiungo mshambuliaji kamili ( kifucho ) . Majukumu ya kuchezesha timu yalikuwa ya Niyonzima akibadili mifumo ya pasi uwanjani , kufunga na kufungua uwanja huku Okwi akitoka kucheza kama namba kumi na kucheza huru kulia na kushoto kwenye final third kama kiungo mshambuliaji namba mbili. 4-3-3 inahitaji viungo washambuliaji zaidi ya wawili. Endapo Yanga wataingia uwanjani kumtazama Okwi tu kwenye safu yao ya ulinzi watakuwa wamekosea na wanaweza kuumia . Umakini unahitajika kwa kuwatizama Simba wanapoanza kutoka nyuma kwenye wings na kati ni akina nani wanaenda timu kabla ya kuingia kwenye eneo lao la ulinzi.
Wapo wengi katika kiungo kwa upande wa Simba ; Ndemla huyu mara nyingi huanzia benchi kutokana na uwezo mkubwa wa kuwasoma wapinzani. Mara kadhaa amekuwa mwiba kwa Yanga kwa kutokea benchi na kubadili matokeo . Matokeo ya 3-3 msimu wa Brandts kwa Yanga huyu ndio alikuja kuikoa Simba wakiwa nyuma kwa goli tatu sambamba na Lucian. Kichuya kulia ni viungo James Kotei na pacha wake Jonasi Mkude ambaye amerudi vyema katika kiwango chake ni watu ambao wanaweza kuichachafya Yanga eneo la kati.
Kwenye ushambuliaji driving force kubwa ya Simba inaanzia kati na kwenye wings . Erasto Nyoni kulia na Zimbwe junior kushoto wana uwezo mkubwa kupanga mashambulizi sambamba na viungo wa pembeni Shiza Kichuya na Haruna Niyonzima ili kuwalisha vyema wachezaji wa kati Emanuel Okwi , Mavugo na Juma Luizio . Yanga kwa sasa si imara sana kwenye wings kama misimu miwili ya nyuma kutokana na kuondokewa na nyota wake kadhaa. Pengo la Saimoni Msuva kulia bado ni kubwa ambaye alikuwa akiwakaba wapinzani kwa kuwashambulia muda wote . Pius Buswita ana kazi ya ziada kuzima kazi ya Zimbwe na Niyonzima kwa jumamosi ili kuwanyima fursa kupitia kwenye wings.
Mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kuondoka kocha msaidizi Jakson Mayanja na ujio wa mburundi Masoud Djuma siyapi sana nafasi kuleta badiliko kubwa hususani kimbinu lakini yanaongeza hamasa ya upambanaji bado Simba itatembelea mipango na mbinu za Omog kuliko Masoud ambaye ni kocha msaidizi na bado hajapata muda wa kutosha na timu.
YANGA SC
Baada ya kuitazama Simba SC kiundani sasa tuwaangazie mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara ambao ndio watakuwa wenyeji wa mechi hiyo dhidi ya mahasimu wao Simba SC.
Kama ilivyo Simba, Yanga pia wanaingia katika mechi hii wakiwa na mtaji mzuri kisaikolojia , kimbinu , kiufundi, ari ya kupambana na hamasa kubwa ya kulinda heshima yao ya soka nchini kama mabingwa mara tatu mfululizo pia wakitaka uongozi wa ligi baada ya kulingana pointi sawa na Simba lakini Simba wakiongoza ligi kwa tofauti ya magoli ya kufunga .
LWANDAMINA
Huyu ndio kocha mkuu wa Yanga ambaye anaingia kwenye mtanange huu akiwa na pressure kubwa kushinda mechi ya derby baada ya kucheza mechi tatu na kuambulia patupu baada ya kufungwa mechi tatu. Lwandamina msimu wa 2016-17 alianza na kupoteza 2-1 na Simba SC. Kwenye michuano ya Mapinduzi alifungwa na Simba kwenye mikwaju ya penati hatua ya nusu fainali baada ya kutoka sare ya 0-0 ndani ya dakika 90. Lwandamina na vijana wake katika mechi ya ufunguzi ligi kuu msimu wa 2017-18 al maarufu kama Ngao ya jamii alipoteza pia kwa mikwaju ya penati hali inayomfanya kabla ya mechi ya jumamosi kuwa na rekodi ya kufungwa mechi tatu na Simba SC na kuambulia sare moja!.
Rekodi hiyo inamfanya George Lwandamina kuingia kwenye Kariakoo Derby akiwa na pressure kubwa kuhitaji matokeo chanya ili kuwaaminisha wapenzi na wanachama wa timu hiyo uwezo wake wa kucheza mechi za Derby kama alivyokuwa Zambia na kikosi cha Zesco United. Umakini , uwezo wa kuisoma Simba , kuandaa vyema kikosi chake ni vitu pekee ambavyo vinaweza kumfanya kushinda mchezo huo na kujipa thamani mpya mbele ya wanachama . Raha ya ubingwa kwa timu hizi mbili ni mmoja kumfunga mwenzake .
Kifalsafa Lwandamina ni muumini mzuri wa soka la kushambulia linalochezwa kwa pasi fupi fupi zenye kasi zikihama kutoka box moja kwenda jingine kwa njia ya kati ambayo inawatumia walinzi wa kati , viungo wa kati na mshambuliaji kiongozi nyuma ya playmaker wa juu anaetengeneza daraja kati ya viungo na mshambuliaji wa kati. Aliwapumzisha Kelvin Yondani na Juma Abdul mchezo wa juzi dhidi ya Stand United kutokana nakuwa na kadi mbili za njano. Kama wangepata kadi kwenye mechi ile ni dhahiri mchezo wa jumamosi wangeukosa ! . Lwandamina humtumia Yondani kama mlinzi kiongozi wa kati ambaye ana uwezo wa kukaba na kushirikiana vyema na kiungo wa chini kuanzisha mashambulizi aidha kupiga mipira mirefu kwenye wings ( fast break / outer ) au give and go passes kuwatafutia mwendo viungo wa kati . Yondani anaetengeneza kombinesheni nzuri na sweeper Vincent Andrew pia ana uwezo wa kuwapanga vyema walinzi wa pembeni aidha kwenye mtego wa kuotea au kufanya marking hususani kuziba njia kabla ya mpira kufika.
Lwandamina ambaye msimu uliopita akiwa na Juma Mwmbusi kama kocha wake msaidizi aliyempokea toka Hans van der Pluijm , aliendeleza falsafa ya kushambulia kupitia pembeni kupitia mawinga kama Saimoni Msuva ambaye hivi sasa ametimkia Al jadida ya Morocco pia Deusi Kaseke wing ya kushoto. Lakini msimu huu baada ya mabadiliko makubwa ya kikosi hicho kwa wachezaji wengi kuondoka na wapya wengi kuingia , Lwandamina amebadili mifumo na mbinu zake kulingana na aina ya wachezaji alionao . Ukiitazama Yanga hivi sasa si timu ambayo inategemea tena wings kutafuta magoli. Yanga inaweka soka chini ambalo linasonga mbele kwa kutandaza mpira chini kutoka box moja kwenda jingine. Katika mechi 5 za awali ligi kuu msimu huu timu ilionekana kukosa kasi , uchache wa kutengeneza nafasi za kufunga pia ubutu wa safu ya ushambuliaji kufunga. Mechi mbili za mwisho dhidi ya Kagera Sugar na Stand United, timu imekuwa na nguvu , kasi , uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga na kufunga huku mfumo ukiruhusu kila mchezaji kucheza kwa uhuru na kujituma. Katika mechi mbili za mwisho Lwandamina akitumia 4-3-3 amepata magoli 6 ! akiwachapa Kagera 2 na kushinda 4-0 dhidi ya Stand United.
Eneo la kiungo amelifungua kunyumbuka katika kujenga mashambulizi pia kuilinda timu katika kushambuliwa. Pappy Tshishimbi licha ya kusimama kama kiungo mkabaji lakini takribani mechi mbili anamtengeneza kama kiraka akiwa uwanjani . Anatibua mipango ya wapinzani kuanzia juu, hushuka chini kukaba lakini pia hutanua kiungo kujilinda kwenye wings ili kuwakataa wapinzani kupitia pembeni ‘ huru’ kushambulia. Mechi na Kagera alimpanga juu kama kiungo mchezeshaji lakini na majukumu mawili kuhakikisha kiungo cha wapinzani wao hakisogei , hakitulii kupanga timu , kumsaidia Makapu kwenye blocking pia kumzunguka Ajibu acheze huru kwenye final third kama ‘ screening ‘ kwenye attacking pattern ndio maana kuna wakati Tshishimbi alikuwa anafanya driving kwenye final third ili Chirwa na Ajibu wafunguke kitu ambacho kilikuwa kinawafanya Stand kurudi nyuma sana na kuvuka kwenye marking zone yao. Hili pia siku ya jumamosi inawezeka akicheza na Rafael Daudi au Kamsoko kama atakuwa amepona.
Piusi Buswita ni mtaji mwingine kwa Lwandamina kwenye wings , hachezi kama winga teleza Saimoni Msuva kwa maana ya ‘ sprinting ‘ . Buswita kulingana na mfumo wa Lwandamina kwa sasa unaotumia pasi fupi fupi ( box to box ) anachezeshwa kama kiungo mchezeshaji wa pembeni anaeukata uwanja anaposhambulia kwa maana ya kuongeza mashambulizi makali ya kati kuwazunguka Ajibu na Chirwa sasa hili huwalazimisha wapinzani hususani walinzi wa pembeni kusogea kati na kuziacha wazi flanks ambazo Ajibu au Chirwa hutanua pembeni kwa ajili ya counter . Simba wasipokuwa makini na mfumo huu kuna uwezekano mkubwa wa Yanga kucheka na nyavu.
Driving force ya Ajibu ambaye kwa sasa anachezeshwa kama mshambuliaji mchezeshaji ( playmaker ) ina faida kubwa kwa Yanga kutengeneza set pieces au ku unlock muhimili wa ulinzi kutokana na uwezo mkubwa wa kukokota mpira pia kuuficha mpira. Licha ya uimara wa kiungo cha chini cha Simba SC lakini bado sio wazuri sana kukabia juu au kuvunja mipango ya wapinzani kabla haijafika kwenye attacking zone , endapo wakimruhusu Ajibu na back up ya viungo wa kati na pembeni kuwa huru kwenye eneo lao la ulinzi hakika Yanga inaweza kucheka na nyavu kwa kuutazama mchezo wa Simba dhidi ya Mtibwa waliopata shida kuwazuia kwenye eneo lao la mwisho.
Wing ya kulia ya Simba SC kama atapangwa Erasto Nyoni na Shiza Kichuya , Lwandamina kuna uwezekano mkubwa wing yake ya kushoto kuendelea kumwamini Gadiel Michael na Mwashiuya ambayo kwenye edge juu wanapata sapoti ya Ajibu kwenye attacking patterns huku kwenye marking Tshishimbi kama kiungo kiongozi kati hufika kutibua au kuziba njia . Erasto mzuri kupanda na kushuka hivyo ni lazima wing iwe technical weight kubwa kumlazimisha kubaki chini kitu ambacho Lwandamina anakiweza kwa kufanya swtiching za namba mara kwa mara kati ya Ajibu , Chirwa na Mwashiuya kwenye pressing .
Sina shaka na uwezo wa Youthe Rostand kwenye lango la Yanga . Ana uwezo mzuri kucheza krosi na kucheza one against one. Kikubwa lazima aongee na walinzi wake wa kati kuziba vyema njia ya kati ambayo kinara wa mabao ligi kuu Emanuel Okwi ni fundi wa kuitumia. Wakiweza kumzuia Haruna Niyonzima kuchezesha timu na kuficha mipira pia wakimziba Mzamiru au Ndemla kulingana na seletion ya Omog basi watamfanya Okwi acheze chini zaidi kama deep playmaker kitu ambacho kitawafanya Yondani na Dante kuwa huru kama wataanza katika pacha hiyo.

0 comentarios:

Publicar un comentario

CCM ZANZIBAR YAIFARIJI FAMILIA ILIYOPATA AJALI YA MOTO NA KUFARIKI WATU WANNE.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akiwafariji ndugu na jamaa wa marehemu wa familia iliyopata msiba huo katika k...